Friday, August 20, 2010

WAGOMBEA WA CHADEMA GEITA WAFANYIWA VITUKO


MWENYEKITI wa Chama Cha Maendeleo na Demokrasia (Chasema) Wilaya ya Geita Mabura Kachoji amewashutumu wafuasi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa wanawafanyia fujo wagombea udiwani wa chama chao.

Akizungumza na Mwananchi mwenyekiti huyo alibainisha kuwa wafuasi hao wamewafanyiwa fujo wagombea wao wawili na kwamba mgombea udiwani wa kata ya Rwamgasa Jimbo la Busanda Ntalima Masawe Paulo alichomewa Nyumba yake.
Kachoji alidai mbali na kuchomewa nyumba kwa mgombea huyo, Mkuu wa Wilaya ya Geita Philimon Shelutete amekuwa akimkamata Mgombea huyo na kumfuga kwa madai ya kukwamisha shughuli za kimaendeleo.

Alieleza Paulo ametiwa ndani kwa amri ya mkuu huyo wa Wilaya mara tatu na kusababisha ashindwe kufuatilia shughuli za maendelo ya kata yake ambayo anagombea.

“Mimi sidhani kama kuna mtu anaweza kukwamisha shughuli za maendeleo hususani katika eneo ambalo anaishi na wakati huo huo, wananchi wa sehemu hiyo wakiwa wanamunga mkono awe kiongozi wao,”alisema Kachoji.

Alisemja Paulo ni mgombea mwenye sifa ya kuwa kiongozi na anaweza kutetea masilahi ya wananchi na kuleta maendeleo kwa wananchi.

Katika tukio lingine, mgombea wa Kata ya Nyamgusu alivamiwa nyumbani kwake na watu wasiojulikana na kumjeruhi kichwani baada ya kumpiga na nondo.

Kitendo hicho, kimemuathiri mgombea huyo kisaikolojia na amejitoa katika kinyanganyiro na chama kililazimika kumsimamisha mgombea mwingine kupitia Chadema.

Katika hatua nyingine ambayo inaonekana kuwa CCM imedhamiria kuwangoa wapinzani ni kitendo cha baadhi ya maofisa watendaji kufunga ofisi zao mara kwa mara pindi wanapogundua kuwa wagombea wa Chadema wanaenda katika ofisi zao kupata huduma.

Alisema matukio hayo yamekuwa ya kawaida kwa maofisa hao na mtendaji wa Kata ya Katoma alifanya kitendo hicho makusudi cha kutoka nje ya ofisi ili kumkwamisha mgombea wa Chadema wakati alipokuwa akirudisha fomu.

Alisema kutokana na hali hiyo, walifanya kazi ya ziada ya kumtafuta kwa njia ya simu ili waweze kupata huduma, lakini mtendaji huyo aliweka vikwazo vingi kama vile hana usafiri wa kumpeleka ofisini

“Kwa kuwa sisi tulikuwa na shida ilibidi tumfuate na usafiri wa pikipiki tuliokuwa nao,na tulipofika aligoma kupanda pikipiki hiyo kwa madai pikipiki ilikuwa na bendera ya Chadema. Lakini tulipomtishia kuwa tutapeleka malalamiko kwa Mkurugenzi wa Manispaa alikubali kupanda pikipiki,”alisema Kachoji.

Kachoji ilibidi atoe taarifa kwa Mkurugenzi wa Wilaya ya Geita Mpangalakela Katala na mkurugenzi huyo aliahidi kufuatilia malalamiko hayo. Habari hii, imeandikwa na Sheilla Sezzy,Geita

1 comment: