Wednesday, August 4, 2010

MREMA ASHANGILIA KIMARO KUANGUSHWA VUNJO


MWENYEKITI wa Tanzania Labour Party (TLP), Agustino Mrema, jana alitembea zaidi ya kilometa 10 kwa miguu kuudhihirishia umma kuwa ana afya nzuri wakati akienda kuchukua fomu za kugombea Ubunge katika Jimbo la Vunjo.


Mrema akiwa na mgombea urais kupitia tiketi ya chama hicho,Mutamwega Mganywa, walitembea kwa miguu kutokea Kijiji cha Chekereni hadi mji mdogo wa Himo,huku akisindikizwa na mamia ya wanachama.

Wanachama hao wakiwa wamevalia fulana za njano zenye nembo ya TLP na maneno "Vunjo hatudanganyiki", walikuwa wakishangilia na vijana waliokuwa wakiendesha pikipiki zaidi ya 40, wakifanya vituko mbalimbali kama ishara ya kushangilia.

Mrema aliwapongeza wanachama wa CCM wa Jimbo la Vunjo kwa kuamuangusha Mbunge aliyemaliza muda wake, Aloyce Kimaro katika kura za maoni.

"Wana-CCM Vunjo ni watu wazuri sana hongereni kwani mlichokifanya ni jambo zuri la kumuondoa Kimaro. Kimaro ana fedha nyingi hivyo, angenisumbua sana,"alitamba Mrema.

Katika mchakato wa kura za maoni, Wakili na Mwanasheria wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii(NSSF), Chrispin Meela aliongoza kwa kupata kura 7,732 dhidi ya Kimaro aliyepata kura 3,207 na hivyo kushindwa kutetea kiti chake.

No comments:

Post a Comment