Raia wa Kenya Nathan Mutei (kushoto) jana amefungwa miaka tisa gerezani au kulipa faini ya Sh 80 milioni baada ya kupatikana na hatia ya kusafirisha albino kutoka Kenya kwa lengo la kumuuza Sh 400 milioni. Mtuhumiwa aliondoka Kitale nchini Kenya Agosti 12, mwaka huu na kuingia Tanzania kupitia mpaka wa Isibania kwa ajili ya kumuuza.
Mutei alipofika Tanzania alionana na mganga wa jadi na baadaye taarifa zilitolewa kwa maofisa wa jeshi la polisi kwamba kuna jamaa anauza albino akiwa hai. Kutokana na taarifa hizo, mtuhumiwa alikamatwa na jeshi hilo na baadaye kushtakiwa na kupatikana na hatia.
Mutei alihukumiwa na Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoani Mwanza, Angelous Rumisha baada ya kukiri makosa yake katika mahakama hiyo.
Katika kosa la kwanza, Mutei alidaiwa kumsafirisha binadamu kinyume na sheria namba 6 ya mwaka 2008 ya makosa ya kusafirisha binadamu.
Kosa la pili, mtuhumiwa anadaiwa kumteka mtu na kutaka kumuua na kuuza viungo vyake kinyume na kanuni za makosa ya adhabu namba 248 kifungu cha 16. Picha na Frederick Katulanda.
No comments:
Post a Comment